NI Wikiendi nyingine tunapokutana kwenye ukurasa huu mzuri. Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu unaendelea na majukumu yako vizuri. Siku chache zilizopita, nilitembelewa na mmoja kati ya wasomaji wangu wa siku nyingi. Sitamtaja jina, lakini kwa sababu kinachomsumbua kimekuwa ni tatizo kwa wanawake wengi, ningependa tujadiliane kwa pamoja. Alichoniambia dada huyu ni kwamba, kwa kipindi kirefu amekuwa akililia bahati ya kuolewa bila mafanikio. Wanaume anaokutana nao, licha ya kumpa ahadi kemkem, wengi wamekuwa wakiishia kumuumiza na kumuacha kwenye mataa.
Anaona umri unakwenda, wadogo zake wote wameshaolewa, wasichana wa rika lake tayari wapo kwenye ndoa zao, lakini yeye yupoyupo tu. Kwa kumtazama, ni msichana mrembo na pengine anawazidi kwa vingi wanawake wengine ambao tayari wapo kwenye ndoa, sasa tatizo ni nini? Anakwama wapi?
Bila shaka, wapo wanawake wengi wanaopitia kipindi kigumu kama dada huyu. Kwa mila za Kitanzania, heshima ya mwanamke inakamilika pale anapoolewa. Hata kama mwanamke atakuwa mrembo vipi, atakuwa na kazi nzuri na uwezo wa kumudu maisha yake, kama atakuwa anaishi bila ndoa, jamii haitampa heshima anayostahili.
Zipo sababu nyingi zinazoweza kumfanya mwanamke akachelewa kuolewa au akakosa kabisa mwanaume wa kuishi naye, kwa maana ya mume wa ndoa. Wanawake wengi wanapoingia kwenye umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea bila ndoa, hupatwa na msongo mkubwa wa mawazo, hujiona kama wana nuksi maishani na wengine hufikia hata hatua ya kwenda kwa waganga kusafisha nyota zao.
Jambo ambalo linaongoza kufanya wanawake wachelewe kuolewa au pengine wasiolewe kabisa, ni aina ya maisha waliyochagua kuishi. Yawezekana ukawa mrembo kwelikweli, sura nzuri, shepu nzuri, kazi nzuri, maisha ya kisasa, lakini ukashangaa huolewi, siku zinazidi kuyoyoma tu. Kama na wewe ni miongoni mwa watu wa aina hii, usijilaumu sana, usijione una mkosi, kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyachunguza na kuyafanyia kazi, baada ya muda mfupi utaona matokeo yake.
UNAPENDA SANA STAREHE?
Hakuna mwanaume anayependa mwanamke mpenda starehe, anayeshinda kwenye kumbi za starehe, anayekesha kwenye ulevi ambaye kwenye kila sherehe hakosekani. Mwanamke anatakiwa kuwa na maisha ya kawaida, ndivyo mila za Kitanzania zinavyotufundisha, ukienda tofauti, kila mwanaume ataanza kukuogopa. Achana na maisha ya anasa kwa sababu starehe zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo.
MAVAZI YAKO YAPOJE?
Hili pia ni tatizo lingine. Mwanamke anaweza kuwa na sifa zote za kuolewa, lakini kwa sababu ya aina ya mavazi anayopendelea kuvaa, wanaume wakawa wanamuogopa au kumtafsiri vibaya. Yapo mavazi ya staha yanayoweza kumfanya mwanamke akaonekana mtu wa heshima mbele ya jamii na kumuongezea mvuto.
Tabia ya kuvaa vi-skin tight vinavyokuchora maumbile yako, sketi fupi zinazoacha maungo yako muhimu wazi na mavazi mengine ya ajabuajabu, itakufanya uwe kivutio cha wale wanaume wanaotaka kutimiza haja za mioyo yao tu, lakini siyo mwanaume anayetaka kuanzisha maisha na mwanamke.
UNA UVUMILIVU KIASI GANI?
Hiki ni kigezo muhimu sana wanachokitumia wanaume wanapotafuta mwanamke wa kuoa. Sifa ya mwanamke ni uvumilivu katika kila jambo. Kama unashindwa kumvumilia leo kwa sababu hana uwezo wa kukuhudumia vizuri, usitegemee anaweza kuja kukuoa.
Wengi hupenda kuwa na wanawake ambao hata wakiingia kwenye ndoa maisha yakayumba, watakuwa tayari kushindia ‘chai na mkate’ na kutunza siri. Mwanaume anapenda mwanamke mvumilivu, hata ikitokea wamegombana leo, atavumilia ili wapate suluhu na siyo kukimbia!
No comments:
Post a Comment