MIGOGORO ya wapendanao kwa sasa imekuwa mingi. Ripoti mbalimbali zinaonesha kwamba kuna anguko kubwa la watu kupeana talaka, watu wanashindwa kuendelea na safari waliyoianzisha kutokana na kushindwana tabia. Hii yote inatokana na mambo mbalimbali ikiwemo maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na mambo ya kuiga. Watu wanakosa msimamo na kujikuta wameingia kwenye mahusiano tofautitofauti bila kujali madhara yake. Ndugu zangu, namna bora ya kuishi vizuri kwenye uhusiano wako kwanza kabisa ni kujitambua. Unapaswa kujua wewe ni nani na unataka kuwa nani maishani. Usiishi bila ya kuwa na malengo.
Bahati mbaya sana wengi wetu tumekuwa tukiishi kama gari bovu. Tunaenda bila kujua tunaelekea wapi katika masuala ya uhusiano. Jitambue wewe ni nani na unahitaji kuwa na mwenza wa aina gani. Unahitaji kuwa na mtu mwaminifu, mkweli na mcha-Mungu? Utampataje?
Nisizu-ngumzie sana eneo la utampataje lakini ninachotaka kuzungumza nawe leo ni juu ya suala zima la kuishi na yule ambaye unaamini ni mtu ambaye anakufaa. Ukiwa una uhakika ni mtu anayekufaa, tumia mbinu hizi ili uweze kuishi kwa amani na furaha.
KUWA MKWELI
Hakuna kitu kizuri sana kwenye masuala ya uhusiano kama kuwa mkweli. Unapo-mueleza ukweli mwenza wako, akiwa muumini wa ukweli basi mtaelewana sana. Ukweli utakuwa unawaweka huru, hamdanganyani kama watoto wadogo.
Tatizo moja hapo huwa linakuja kama mwenzi wako naye si mtu wa kupenda ukweli. Itabidi pia ufanye kazi ya ziada ya kumuelimisha maana wapo watu ambao wao wakiambiwa ukweli huwa hawafurahii, wanapodanganywa au kupewa ahadi tamutamu hata kama ni za uongo wao huzifurahia.
KUTOCHUNGANA
Kuchungana sana huwa nalo ni tatizo. Simaanishi kwamba usimfuatilie mwenza wako lakini isizidi sana mpaka ikageuka kuwa kero. Mpe nafasi ya kufanya mambo yake kwa uhuru, mtengenezee mazingira ya kujiamini na kukuamini pia. Kikubwa hapa kila mmoja wenu anatakiwa tu kujitambua kwamba yeye ni mtu mzima, afanye mambo kama mtu mzima. Ajue kwamba mwenzake amemuamini hivyo asifanye mzaha wa aina yoyote ambao unaweza kumvunjia heshima yake.
Usijirahisi kuingia kwenye mtego wa walaghai wa mapenzi. Mtunzie heshima mwenza wako ukiwa na imani kwamba hata yeye anakutunzia. Ishi maisha yenye nidhamu kama vile mwenzako anakuona kila uendako. Chunga usisaliti. Usaliti haujawahi kumuacha mtu salama, ipo siku utabainika na kuaibika.
HESHIMIANENI
Mkiheshimiana kwenye mahusiano mambo yatakwenda vizuri. Kila mmoja amheshimu mwenzake. Asimdharau, amuone kwamba ana umuhimu katika safari yake. Mwanaume ajue kabisa anamhitaji mwanamke wake maishani. Vivyo hivyo mwanamke, amheshimu mwanaume wake. Ampe nafasi kubwa maishani mwake kuliko mwanaume mwingine yeyote. Mkizingatia hayo, mtayafurahia maisha. Mtapeana thamani, kila mmoja atajivunia kuwa na mwenzake.
KURIDHIKA
Unapotafuta mwenza wa maisha, hakikisha kweli unampata ambaye atakufanya uridhike kwa maana ya sifa na tabia njema. Ukishampata huyo, ridhika. Kila unayekutana naye, muweke daraja la pili. Amini kwamba mtu wako ndiye bora kuliko mwingine yeyote
No comments:
Post a Comment