NI Ijumaa nyingine ninapokukaribisha mpendwa msomaji wangu kwenye ukurasa huu murua. Siku chache zilizopita, nilipata bahati ya kuzungumza na msomaji wangu mmoja aliyepo Morogoro, sitalitaja jina lake kwa sababu maalum.
Alikuwa akihitaji ushauri na kubwa linalomsumbua, ni kwamba anajihisi hana bahati katika maisha yake ya kimapenzi. Kila mwanaume anayekutana naye, anaishia kumchezea na kumuacha njiani.
Wasichana wa rika lake wote wameshaolewa, wengine walishajenga familia na wengine wapo kwenye hatua ya uchumba rasmi, lakini yeye ni mtu wa kulia na upweke kila siku, akimpata mwanaume wanakaa baada ya muda fulani kisha anaanza kumuonesha kumuonesha mabadiliko makubwa ya tabia na mwisho wanaishia kuachana.
Sasa anajihisi umri unaenda, ameshachoshwa na upweke, anahitaji mwenza wa kuanzisha naye familia, ambaye atampenda na kumheshimu lakini hajui atampata vipi au atamjuaje kama ni mkweli au ndiyo walewale?
Huenda dada yangu huyu anawakilisha wanawake wengi huko mitaani ambao licha ya kujaliwa kila kitu, bado wameendelea kuteseka na upweke, wanaishia kutumiwa tu na kuachwa, wengine wanajikuta wakizalia nyumbani na kuendelea kuzisikia ndoa kwenye bomba.
Tunakubaliana kwamba suala la ndoa ni bahati, unaweza kuwa unalalamika kwamba hupati mtu wa kukuoa, lakini kuna mwanamke mwingine ameshaolewa zaidi ya mara tatu na wanaume tofauti na kuachana nao.
Anaolewa, anaachika. Baada ya muda fulani anaolewa tena, anaachika na mtiririko unakuwa ni huo. Unaweza kujiuliza, kwa nini mwingine apate bahati ya kuolewa mara mbili au tatu kwa nyakati tofauti, wakati kuna mwingine hajawahi kabisa kuolewa na mpaka sasa hakuna dalili?
Ukiwauliza wanaume ambao hawajaoa wanapenda kuwaoa wanawake wa aina gani, utashangaa kwamba watapishana kidogo kwenye sura na mwonekano, lakini mambo mengine yote yatakuwa yakifanana. Sifa atakazokuwa anazitaka Juma kwa mke atakayemuoa, hazitapishana sana na sifa anazozitaka Hamis na ndizo hizohizo anazozitaka Mohamed.
Lakini bahati mbaya wakati wanaume wakiwa na vigezo vyao, wanawake wengi hawajui namna ya kujiweka ili mwanaume asiishie kutembea naye kwa mwezi mmoja au miwili kisha akamuacha.
Na hapa ndipo unapokuta wanawake wanatumia muda mwingi nyuma ya vioo, kujipamba, kujipodoa, wanashinda saluni, wanatumia vipodozi vikali, wakati mwingine vinawasababishia madhara makubwa. Wanachokiamini wao, wakipendeza itakuwa ni rahisi kuwapata wanaume wa kuwaoa. Hata hivyo, wapo ambao licha ya juhudi zote za kupendeza wanazozionesha, bado wanajikuta wakiendelea kusota bila ndoa.
Ndoa siyo jambo la mchezo, hadi mwanaume aamue kwamba kweli huyu anafaa kuwa mke, ni lazima awe amekupitisha kwenye chujio kali bila wewe mwenyewe kujua. Upo naye, lakini mwenzako anakusoma, kila unachokifanya anajaribu kukitathmini kwa kina, akiona huelekei, mwisho anakuacha na kumuoa msichana mwingine wa mtaani.
Sasa swali la msingi unalopaswa kujiuliza ewe dada au mwanamke, ni wapi unapokosea hadi ndoa inaendelea kuwa msamiati mgumu kwako? Nitumie majibu yako na wiki ijayo nitakupa siri zinazowafanya wengine wanaolewa mara kadhaa huku wengine wakizeeka bila kupata ndoa
No comments:
Post a Comment