MUNGU ni mwema sana, ni Jumatatu nyingine tunakutana kwenye eneo hili maridhawa la kupeana darasa kuhusiana na masuala ya uhusiano. Leo nitazungumza zaidi na wanaume lakini ni vizuri pia wanawake wakasoma ili kuwaweka sawa wanaume wao. Yawezekana asisome mwanaume wako lakini ukimpelekea nakala ya ukurasa huu, hakika atajifunza makosa yake ili awaze kujirekebisha na mwisho wa siku penzi lenu litastawi na mtafurahia mahaba kila uchwao.
Baadhi ya wanaume huwa wanajisahau kufanya wajibu wao kwa kisingizio cha majukumu ya kikazi, wakati mwingine hutumia kisingizio hicho kufanya mambo yasiyofaa na wakirudi kwa wenza wao wanashindwa kuwatimizia haja zao. Wakati mwingine kitendo tu cha mtu kujiona mwanaume, anaamini yeye ni kiongozi. Anaamini kwamba hawezi kukosea na kwamba neno lake linakuwa ndio sheria katika nyumba, kitu ambacho si sahihi. Lugha za amri, kutoa matamko wanafikiri ndio sawasawa bila kujua wanafanya makosa.
Ndugu zangu, ni vyema tukajifunza baadhi ya makosa ambayo wanaume wamekuwa wakiyafanya mara kwa mara ambayo husababisha uhusiano uyumbe. Uhusiano unapoyumba ndipo mianya ya usaliti inapofunguka na mwanamke kujikuta amesaliti.
UBABE
Wanaume wengi wamekuwa wakitumia ubabe sana kutokana na asili bila kujua kwamba ubabe unaposhamiri katika uhusiano, unaondoa ladha ya mapenzi. Ubabe unamfanya mwenzi wako akose amani, unaondoa ile hali ya mashamsham ya mapenzi.
Unashauriwa kupunguza ubabe kwa mwenzi wako. Hata kama jambo limekukasirisha, kuna namna ambayo unaweza kumuonesha na yeye akaelewa kwamba hujapendezwa na jambo fulani. Wengi wetu tunafahamu hata katika familia ambayo baba anakuwa mkali kupitiliza, watoto wanaishi kwa hofu. Badala ya kumheshimu, watoto wanamuogopa baba. Haitakiwi mke au mchumba wako akuogope kiasi hicho. Anapaswa kukuheshimu kama mpenzi wake na si kukuogopa. Anapaswa kukuona rafiki yake na si kama mtu na bosi wake.
KUTOMUUNGA MKONO
Wanaume wengi huwa na ‘kakiburi’ fulani hivi ambako mara nyingi hujikuta wakiwafanyia dharau wanawake zao kwa kujua au kutokujua. Wanashindwa kuwaunga mkono katika mambo yao. Wakati mwingine hata katika mazungumzo, mwanaume anamsikiliza mwanamke wake halafu anampotezea. Anaona kama vile vitu anavyomwambia ni vya kijinga au vya kitoto. Anamsikiliza tu na kuachana naye, anaendelea na shughuli zake nyingine. Hata kama mke ana biashara, ana wazo la biashara labda pengine ameamua kumshirikisha, mwanaume hajali. Anaona biashara ni zile anazofanya yeye na si mkewe.
Hili ni kosa kubwa sana ndugu zangu, muunge mkono mwenza wako hata kama unaona jambo analokushirikisha halina maana sana. Wanawake wanapenda kusapotiwa na wanaume zao, ndio maana wale mafundi wa kuwasapoti wanawake, wanapowafanyia hivyo hata wake za watu wanaingia mkenge.
MAZOEA YA TENDO
Wanaume wengi wanapokuwa wameishi na wenza wao kwa muda mrefu hususan wanandoa, huwa na kasumba ya kujisahau. Wanachukulia suala la tendo la ndoa kwa wake zao ni jambo la bahati mbaya tu. Linatokea siku ikitokea na si lazima sana. Burudani wanaipata nje ya ndoa. Ndugu zangu, pamoja na kumuonesha upendo, kumjali mkeo bado unapaswa kulitenda tendo la ndoa kikamilifu. Unapaswa kumkata kiu yake na si kumuacha hewani.
NYONGEZA…
Wanaume wengi wana kasumba ya kutokuwabembeleza wenza wao. Mbembeleze mwanamke wako, mfanye ajione wa pekee, mpe lugha tamu na za kumpa matumaini mapya. Mdekeze ikibidi, usimuonee aibu. Mpe maneno mazito ya kimahaba mnapokuwa wawili, mueleze kwamba una hamu naye, unainjoi akikufanyia nini na kadhalika. Kwa leo inatosha.
Usisahau kushare post hii. Share facebook, twitter, Google+ n.k bila kusahau WhatsApp! Share kote wenzio nao wasome
No comments:
Post a Comment